Ufumbuzi wa Programu ya Family Link kwa Wazazi wenye Watoto walio na umri wa chini ya miaka 13 (au umri unaoruhusiwa katika nchi uliko)

Angalia Ilani ya Faragha kwa Wasifu na Akaunti za Google Zinazodhibitiwa kupitia Family Link, za Watoto walio chini ya umri wa miaka 13 (au umri uliobainishwa katika nchi yako)

Karibuni Wazazi!

Imani unayotuonyesha ni muhimu sana kwetu na tunafahamu kwamba kumruhusu mtoto wako awe na Akaunti ya Google ni uamuzi mkubwa. Chukua muda kidogo ukague maelezo haya muhimu ili upate maelezo zaidi.

Akaunti ya Google ya mtoto wako

Akaunti ya Google ya mtoto wako inafanana na akaunti yako na inamruhusu afikie bidhaa na huduma nyingi za Google, ikiwa ni pamoja na huduma ambazo hazijabuniwa au kurekebishwa kwa ajili ya watoto. Mtoto wako anaweza kutumia akaunti yake kufanya mambo kama vile:

  • Kuuliza maswali, kufikia na kutafuta kwenye intaneti kwa kutumia programu ya Mratibu wa Google, Chrome na huduma ya Tafuta na Google;

  • Kuwasiliana na wengine kupitia Gmail, SMS, video, sauti na mbinu zingine za mawasiliano;

  • Kupakua, kununua na kufurahia programu, michezo, muziki, filamu na maudhui mengine;

  • Kubuni, kuangalia na kushiriki picha, video, mawasilisho, hati na maudhui mengine;

  • Kufuatilia maelezo ya afya na siha yakiwemo kiwango cha shughuli na mapigo ya moyo katika Google Fit (kulingana na vifaa vya mtoto wako);

  • Kuona matangazo yanayolingana na maudhui anapotumia huduma za Google.

Family Link na usimamizi wa wazazi

Programu ya Family Link kutoka Google imebuniwa ili kukusaidia uweke kanuni za msingi na umwelekeze mtoto wako anapogundua mambo mtandaoni. Mtoto wako atakuwa katika Kikundi cha familia kwenye Google, ambacho unaweza kutumia kushiriki huduma za Google na mtoto wako na hadi wanafamilia wengine wanne. Utaweza kumwongeza mzazi mwingine baadaye ili akusaidie kusimamia akaunti ya mtoto wako. Wazazi wanaweza kutumia Family Link kufanya mambo kama vile:

  • Kuweka vikomo vya muda wa kutumia kifaa kwenye vifaa vya mtoto wako vya Android au vya ChromeOS;

  • Kuona mahali vilipo vifaa vya Android ambavyo mtoto wako amevitumia kuingia katika akaunti;

  • Kuidhinisha upakuaji na ununuzi ambao mtoto wako anafanya kwenye Google Play na Stadia au kudhibiti uonekanaji wa maudhui kulingana na ukadiriaji wa ukomavu;

  • Kumsaidia mtoto wako achague aina za shughuli zinazoweza kuhifadhiwa katika Akaunti yake ya Google na jinsi zinavyoweza kutumiwa kufanya hali ya utumiaji imfae;

  • Kudhibiti mipangilio kama vile Utafutaji Salama katika huduma ya Tafuta na Google;

  • Kukagua idhini za programu za mtoto wako, kama vile uwezo wa kufikia maikrofoni, kamera na anwani kwenye Android na ChromeOS;

  • Kubadilisha mipangilio ya maudhui, ufikiaji na mipangilio mingine kwa ajili ya matumizi ya YouTube (inapopatikana), ikiwa ni pamoja na YouTube na YouTube Kids.

Ingawa vidhibiti vya wazazi kwenye Family Link vinaweza kukusaidia kusimamia na kudhibiti hali ya matumizi ya mtoto wako, kuna vikomo ambavyo unapaswa kuvizingatia:

  • Ingawa vidhibiti vingi vya wazazi kwenye Family Link vinaweza kudhibitiwa katika wavuti, utahitaji programu ya Family Link kwenye Android au iOS ili udhibiti vipengele fulani kama vile vikomo vya muda wa kutumia kifaa.

  • Mipangilio kama vile Utafutaji Salama, vizuizi vya tovuti kwenye Chrome na vichujio kwenye Duka la Google Play inaweza kusaidia kuzuia ufikiaji wa maudhui yasiyofaa, lakini mipangilio si sahihi kabisa. Hata kama umewasha vidhibiti hivi, huenda mtoto wako bado akafikia maudhui ambayo hutaki ayaone.

  • Idhini ya mzazi haihitajiki mtoto wako anapopakua tena programu fulani au maudhui mengine ambayo yaliidhinishwa hapo awali, anaposakinisha sasisho kwenye programu (hata sasisho linaloongeza maudhui au linaloomba data au ruhusa za ziada), au anapopakua maudhui yaliyoshirikiwa kwenye Maktaba yako ya Familia ya Google Play.

  • Baadhi ya vipengele vya Family Link vinapatikana kwa masharti fulani tu na vinahitaji mipangilio au hali mahususi ili vifanye kazi. Kwa mfano, kipengele cha kuzuia programu kinapatikana tu wakati mtoto wako ameingia katika akaunti kwenye kifaa cha Android au ChromeOS kinachooana. Kipengele cha kuona mahali kifaa cha mtoto wako kilipo katika programu ya Family Link kinapatikana tu wakati kifaa chake cha Android kimewashwa na kimeunganishwa kwenye intaneti.

Mtoto wako atakapofikisha umri wa miaka 13 (umri unaweza kutofautiana kulingana na nchi), ataweza kuchagua kudhibiti akaunti yake mwenyewe bila kusimamiwa.

Waheshimu Wengine

Huduma zetu nyingi humruhusu mtoto wako awasiliane na watu wengine wanaozitumia. Tungependa kudumisha mazingira yenye heshima kwa kila mtu. Hali hii inamaanisha kuwa lazima mtoto wako afuate kanuni za msingi za maadili, kama vile kutowatusi au kutowadhuru wengine au yeye mwenyewe (au kutishia au kuhimiza matusi au madhara kama hayo) - kwa mfano, kwa kupotosha, kulaghai, kukashifu, kuchokoza, kunyanyasa, kunyatia wengine, au kwa kusambaza maudhui ya chuki hadharani (kama vile maudhui yanayochochea chuki au ubaguzi kwa misingi ya asili, mbari, dini, jinsia, mwelekeo wa kingono wa watu n.k.) anapotumia huduma zetu. Uchapishaji wa maudhui ya chuki unaweza kukufanya wewe na mtoto wako mwajibike kwa makosa ya jinai au uharibifu.

Faragha ya mtoto wako

Ili mtoto wako aweze kuwa na wasifu au Akaunti yake ya Google, tunaweza kuhitaji ruhusa yako ili tukusanye, tutumie au tufumbue taarifa za mtoto wako jinsi inavyofafanuliwa katika Ilani hii ya Faragha na Sera ya Faragha ya Google. Unapomruhusu mtoto wako kutumia huduma zetu, wewe na mtoto wako mnaamini kuwa tutalinda taarifa zenu. Tunaelewa kuwa hili ni jukumu kubwa na tunajitahidi sana kulinda taarifa zenu na kuwapa udhibiti. Unaweza kuchagua iwapo mtoto wako anaweza kudhibiti vidhibiti vya shughuli zake kwa mambo kama vile Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, Historia ya YouTube na katika maeneo yanayoruhusiwa, kuunganisha huduma fulani za Google.

Ilani hii ya Faragha ya Wasifu na Akaunti za Google Zinazodhibitiwa kupitia Family Link, kwa Watoto walio na umri wa chini ya miaka 13 (au umri unaotumika katika nchi uliko) na Sera ya Faragha ya Google hufafanua desturi za faragha za Google. Ikitokea kuwa kuna desturi za faragha ambazo ni mahususi kwa akaunti au wasifu wa mtoto wako, kama zile zinazohusu vikomo katika utangazaji uliowekwa mapendeleo, tofauti hizo zimebainishwa katika llani hii ya Faragha.

Ilani hii ya Faragha haitumiki kwenye mbinu, vitendo, tovuti na programu za wengine (si Google) ambazo mtoto wako anaweza kutumia. Unapaswa kukagua sera na sheria na masharti yanayotumika ya vitendo, tovuti na programu za wengine ili kubaini iwapo yanafaa mtoto wako, ikiwa ni pamoja na mbinu zake za kukusanya na kutumia data.

Taarifa Tunazokusanya

Ukishamruhusu mtoto wako awe na wasifu au Akaunti ya Google, wasifu au akaunti yake itachukuliwa kwa jumla kama yako mwenyewe kulingana na taarifa tunazokusanya. Kwa mfano, tunakusanya:

Taarifa ambazo wewe na mtoto wako mnatupa au kubuni.

Kama sehemu ya mchakato wa kufungua akaunti au wasifu, huenda tukakuomba taarifa binafsi kama vile jina la kwanza na la mwisho, anwani ya barua pepe na tarehe ya kuzaliwa. Tunakusanya taarifa ambazo wewe au mtoto wako mnaweka, kama vile maelezo ya anwani yako ya mawasiliano mtandaoni, ambayo tunatumia tunapotaka kuwasiliana nawe ili kuomba idhini. Tunakusanya pia taarifa ambazo mtoto wako anabuni, kupakia au kupokea kutoka kwa wengine anapotumia akaunti au wasifu wake, kama vile mtoto wako anapohifadhi picha katika programu ya Picha kwenye Google au anapobuni hati katika Hifadhi ya Google.

Taarifa tunazokusanya kutoka kwa mtoto wako anapotumia huduma zetu.

Huwa tunakusanya na kuhifadhi kiotomatiki taarifa fulani kuhusu huduma ambazo mtoto wako anatumia na jinsi mtoto wako anavyozitumia, kama vile mtoto wako anapoweka hoja katika huduma ya Tafuta na Google, anapozungumza na programu ya Mratibu wa Google au anapotazama video kwenye YouTube Kids. Taarifa hizi ni pamoja na:

  • Programu, vivinjari na vifaa vya mtoto wako

    Tunakusanya taarifa kuhusu programu, vivinjari na vifaa ambavyo mtoto wako anatumia kufikia huduma za Google, ikiwa ni pamoja na vitambulishi vya kipekee, aina na mipangilio ya vivinjari, aina na mipangilio ya vifaa, mfumo wa uendeshaji, maelezo ya mtandao wa simu yakiwemo jina na namba ya simu ya mtoa huduma na namba ya toleo la programu. Tunakusanya pia taarifa kuhusu jinsi mtoto wako anavyotumia programu, vivinjari na vifaa vyake kwenye huduma zetu, ikiwa ni pamoja na anwani ya IP, ripoti za programu kuacha kufanya kazi, shughuli za mfumo na tarehe, saa na URL inayoelekeza ya ombi la mtoto wako. Kwa mfano, tunakusanya taarifa hizi wakati huduma ya Google kwenye kifaa cha mtoto wako inawasiliana na seva zetu, kama vile anaposakinisha programu kutoka kwenye Duka la Google Play.

  • Shughuli za mtoto wako

    Tunakusanya taarifa kuhusu shughuli za mtoto wako katika huduma zetu, kulingana na mipangilio ya akaunti ya mtoto wako, ambayo tunatumia kutekeleza mambo kama vile kumpendekezea programu ambazo huenda akazipenda kwenye Google Play. Unaweza kuchagua iwapo mtoto wako anaweza kudhibiti vidhibiti vyake vya shughuli. Taarifa za shughuli za mtoto wako tunazokusanya zinaweza kujumuisha mambo kama vile hoja za utafutaji, video anazotazama, maelezo ya sauti na matamshi anapotumia vipengele vya sauti, watu anaowasiliana au anaowatumia maudhui na historia ya kuvinjari kwenye Chrome ambayo amesawazisha na Akaunti yake ya Google. Mtoto wako akitumia huduma zetu kupiga na kupokea simu au kutuma na kupokea ujumbe, kwa mfano akitumia Google Meet au Duo, tunaweza kukusanya taarifa za kumbukumbu za simu. Mtoto wako anaweza kwenda kwenye Akaunti yake ya Google ili apate na kudhibiti taarifa za shughuli zinazohifadhiwa kwenye akaunti au wasifu wake na unaweza pia kumsaidia kudhibiti taarifa za shughuli zake kwa kuingia katika Akaunti yake ya Google, au kufikia wasifu wake katika programu ya Family Link.

  • Taarifa kuhusu mahali aliko mtoto wako

    Tunakusanya taarifa kuhusu mahali aliko mtoto wako wakati anatumia huduma zetu. Mahali aliko mtoto wako panaweza kubainishwa kwa kutumia GPS, anwani ya IP, data ya vitambuzi kutoka kwenye kifaa chake na maelezo kuhusu vitu vilivyo karibu na kifaa chake kama vile milango ya mtandao wa Wi-Fi, minara ya mitandao na vifaa vinavyotumia Bluetooth. Aina za data ya mahali tunazokusanya zinategemea kwa kiasi fulani mipangilio yako na vifaa vya mtoto wako.

  • Taarifa za sauti na za matamshi ya mtoto wako

    Tunaweza kukusanya taarifa za sauti na za matamshi ya mtoto wako. Kwa mfano, mtoto wako anapotumia amri za kuwasha kipengele cha sauti (k.m., “OK, Google” au anapogusa aikoni ya maikrofoni), rekodi ya matamshi au sauti itakayofuata itachakatwa ili kujibu ombi lake. Pamoja na hayo, iwapo Chaguo la Shughuli za Sauti na Kutamka la mtoto wako limechaguliwa kwenye mipangilio ya Historia ya Shughuli kwenye Wavuti na Programu, rekodi ya sauti anayotumia katika programu ya Mratibu kwenye kifaa alichotumia kuingia katika akaunti (pamoja na sekunde chache kabla) inaweza kuhifadhiwa kwenye akaunti yake.

Tunatumia teknolojia mbalimbali kukusanya na kuhifadhi taarifa za mtoto wako, ikiwa ni pamoja na vidakuzi, lebo za pikseli, hifadhi ya mfumo, kama vile hifadhi ya wavuti kwenye kivinjari au akiba za data ya programu, hifadhidata na kumbukumbu za seva. Hatumwombi mtoto wako taarifa binafsi zaidi ya zinazohitajika ili kutumia bidhaa na huduma za Google zinazopatikana katika wasifu au akaunti hizi.

Jinsi Tunavyotumia Maelezo Tunayokusanya

Sera ya Faragha ya Google inafafanua kwa kina kuhusu jinsi tunavyoweza kutumia data ambayo Google hukusanya inayohusiana na wasifu au Akaunti ya Google ya mtoto wako. Kwa jumla, tunatumia maelezo ya mtoto wako: kutoa, kudumisha na kuboresha huduma zetu; kubuni huduma mpya; kufanya huduma zetu zimfae mtoto wako; kupima utendaji na kuelewa jinsi huduma zetu zinavyotumika; kuwasiliana moja kwa moja na mtoto wako kuhusu huduma zetu; na kusaidia kuboresha usalama na uthabiti wa huduma zetu.

Tunatumia teknolojia mbalimbali kuchakata maelezo ya mtoto wako kwa madhumuni haya. Tunatumia mifumo ya kiotomatiki ambayo huchanganua maudhui ya mtoto wako ili kumpa huduma kama vile matokeo ya utafutaji yaliyoboreshwa au vipengele vingine kulingana na jinsi anavyotumia huduma zetu. Tunachanganua pia maudhui ya mtoto wako ili tuweze kugundua matumizi mabaya kama vile barua taka, programu hasidi na maudhui yasiyo halali. Pia, tunatumia algoriti ili kutambua mambo yanayofanana katika data. Tunapotambua barua taka, programu hasidi, maudhui yasiyo halali na matumizi mengine mabaya kwenye mifumo yetu, yanayoashiria ukiukaji wa sera zetu, huenda tukafunga wasifu au akaunti yake au kuchukua hatua nyingine inayofaa. Katika hali fulani, pia tunaweza kuripoti ukiukaji huu kwa mamlaka yanayofaa.

Kulingana na mipangilio ya akaunti ya mtoto wako, tunaweza kutumia maelezo yake kutoa mapendekezo, maudhui yaliyowekewa mapendeleo na matokeo ya utafutaji yaliyoboreshwa. Kwa mfano, kulingana na mipangilio ya akaunti ya mtoto wako, Google Play inaweza kutumia maelezo kama vile programu alizoweka mtoto wako ili kupendekeza programu mpya ambazo huenda akazipenda.

Pia, kulingana na mipangilio ya akaunti ya mtoto wako, tunaweza kuunganisha taarifa tunazokusanya katika huduma zetu na kwenye vifaa vyote vya mtoto wako kwa madhumuni yaliyoelezwa hapo juu. Kulingana na mipangilio ya wasifu au akaunti ya mtoto wako, shughuli zake kwenye programu na tovuti zingine zinaweza kuhusishwa na taarifa zake binafsi ili kuboresha huduma za Google.

Google haitaonyesha matangazo yaliyowekewa mapendeleo kwa mtoto wako, hali inayomaanisha kuwa matangazo hayo hayatalingana na maelezo kutoka kwenye wasifu au akaunti ya mtoto wako. Badala yake, matangazo yanaweza kulingana na maelezo kama vile maudhui ya tovuti au programu anayotumia mtoto wako, hoja ya sasa ya utafutaji au maelezo ya jumla ya mahali (kama vile jiji au jimbo). Wakati mtoto wako anavinjari wavuti au anatumia programu zisizo za Google, anaweza kuona matangazo ya watoa huduma wengine wa matangazo (si Google), ikiwa ni pamoja na matangazo ya washirika wengine, ambayo yanamlenga mtoto wako binafsi.

Maelezo Ambayo Mtoto Wako Anaweza Kushiriki

Wakati mtoto wako ameingia katika wasifu au akaunti yake ya Google, huenda akaweza kushiriki maelezo, ikiwa ni pamoja na picha, video, sauti na mahali alipo, hadharani na wengine. Mtoto wako anaposhiriki maelezo hadharani, yanaweza kufikiwa kupitia mitambo ya kutafuta kama vile huduma ya Tafuta na Google.

Maelezo ambayo Google Hushiriki

Maelezo tunayokusanya yanaweza kutumika nje ya Google katika hali chache. Hatushiriki taarifa binafsi na kampuni, mashirika au watu binafsi nje ya Google isipokuwa katika hali zifuatazo:

Ukitupa idhini

Tutashiriki taarifa zako binafsi nje ya Google ukitupa idhini (kama inavyotumika).

Kwenye kikundi cha familia yako

Maelezo ya mtoto wako, ikiwa ni pamoja na jina, picha, anwani yake ya barua pepe na ununuzi aliofanya kwenye Google Play yanaweza kushirikiwa na wanafamilia katika kikundi cha familia yako kwenye Google.

Kwa ajili ya mchakato wa nje

Tunatoa taarifa binafsi kwa washirika wetu au biashara au watu tunaowaamini ili wazichakate kwa niaba yetu, kulingana na maagizo yetu na kwa kutii Ilani hii ya Faragha, Sera ya Faragha ya Google na hatua nyingine zozote zinazofaa za usiri na usalama.

Kwa sababu za kisheria

Tutashiriki taarifa binafsi na kampuni, mashirika au watu walio nje ya Google ikiwa tunaamini kwa nia njema kwamba ufikiaji, utumiaji, uhifadhi au ufichuzi wa maelezo hayo unafaa kiuadilifu katika:

  • kutimiza sheria, kanuni, mchakato wa kisheria au ombi lolote la utekelezaji la kiserikali ambalo linakubalika.

  • kutekeleza Sheria na Masharti yanayotumika, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa ukiukaji unaoweza kutokea;

  • kutambua, kuzuia, au vinginevyo kushughulikia matatizo ya ulaghai, usalama au ya kiufundi.

  • kulinda dhidi ya madhara ya haki, mali au usalama wa Google, watumiaji wetu au umma kama inavyotakikana au kuruhusiwa na sheria.

Tunaweza pia kushiriki taarifa ambazo hazimtambulishi mtu binafsi (kama vile mitindo kuhusu matumizi ya jumla ya huduma zetu) kwa umma na kwa washirika wetu — kama vile wachapishaji, watangazaji, wasanidi programu au wenye hakimiliki. Kwa mfano, tunashiriki maelezo hadharani ili kuonyesha mitindo kuhusu matumizi ya jumla ya huduma zetu. Pia, tunaruhusu washirika mahususi kukusanya maelezo kutoka kwenye vivinjari au vifaa kwa madhumuni ya matangazo na upimaji kwa kutumia vidakuzi vyao au teknolojia kama hizo.

Uwezo wa Kufikia Taarifa Binafsi za Mtoto Wako

Ikiwa mtoto wako ana Akaunti ya Google, unaweza kufikia, kusasisha, kuondoa, kuhamisha na kuzuia uchakataji wa maelezo ya mtoto wako kwa kuingia katika Akaunti yake ya Google. Iwapo hukumbuki nenosiri la mtoto wako, unaweza kulibadilisha kupitia programu ya Family Link au mipangilio ya Family Link kwenye wavuti. Ukishaingia katika akaunti, unaweza kutumia vidhibiti mbalimbali vilivyofafanuliwa katika Sera ya Faragha ya Google, kama vile vidhibiti vya shughuli kwenye Google, ili kusaidia kudhibiti maelezo na mipangilio ya faragha ya mtoto wako.

Iwapo mtoto wako ana wasifu, unaweza kufikia, kusasisha, kuondoa, kuhamisha na kudhibiti uchakataji wa maelezo ya mtoto wako kupitia programu ya Family Link au mipangilio ya Family Link kwenye wavuti.

Mtoto wako atakuwa na uwezo wa kufuta shughuli zake za zamani katika sehemu ya "Shughuli Zangu" na kwa chaguomsingi, kutoa idhini kwa programu za wengine (ikiwa ni pamoja na idhini ya kujua mahali kifaa kilipo, kufikia maikrofoni au anwani). Unaweza pia kutumia Family Link kubadilisha au kurekebisha maelezo ya wasifu au Akaunti ya Google ya mtoto wako, kukagua shughuli na idhini za programu na kudhibiti uwezo wa mtoto wako wa kutoa ruhusa fulani kwa programu au huduma za wengine, ili zifikie maelezo ya mtoto wako.

Iwapo wakati wowote ule ungependa kusimamisha ukusanyaji au utumiaji zaidi wa maelezo ya mtoto wako, unaweza kufuta wasifu au Akaunti yake ya Google kwa kubofya ”Futa akaunti” au “Futa wasifu” kwenye ukurasa wa Maelezo ya Wasifu au Akaunti katika programu ya Family Link au mipangilio ya Family Link kwenye wavuti. Taarifa za wasifu au za akaunti ya mtoto wako zitafutwa kabisa baada ya kipindi fulani adilifu.

Wasiliana Nasi

Kama una maswali yoyote kuhusu wasifu au Akaunti ya Google ya mtoto wako, usisite kuwasiliana nasi. Tuko hapa kukuhudumia. Unaweza kupata maelezo ya ziada kuhusu Family Link na wasifu au Akaunti ya Google ya mtoto wako katika kituo chetu cha usaidizi. Unaweza pia kututumia maoni kuhusu Family Link au wasifu au Akaunti ya Google ya mtoto wako katika programu ya Family Link kwa kugusa Menyu ☰ > Usaidizi na Maoni > Tuma maoni, au kwa kuwasiliana nasi kupitia barua pepe au anwani iliyo hapa chini.

Google
1600 Amphitheatre Parkway
Mountain View, CA 94043 USA
Namba ya Simu: +1 855 696 1131 (Marekani)
Kwa nchi nyingine, tembelea g.co/FamilyLink/Contact

Iwapo una maswali kuhusu jinsi Google hukusanya na kutumia data ya mtoto wako, unaweza kuwasiliana na Google na afisa wetu wa ulinzi wa data. Unaweza pia kuwasiliana na mamlaka ya ulinzi wa data mahali ulipo ikiwa una matatizo kuhusu haki zako kwa mujibu wa sheria za mahali uliko.

Angalia Ufumbuzi wa Family Link kwa Watoto walio na umri wa chini ya miaka 13 (au umri unaoruhusiwa katika nchi uliko)

Programu za Google
Menyu kuu